Yanga yateua 12 kamati ushindi, Kamusoko safi
WIKI tano kabla ya kuanza kwa Ligi Kuu ya soka Tanzania Bara, mabingwa watetezi, Yanga wameunda kamati mpya ya mashindano itakayosimamia timu yao ishinde mechi zake. Hayo yamo katika taarifa ya Yanga iliyotolewa Dar es Salaam na msemaji wao, Dismas Ten aliyesema kamati hiyo itakuwa na wajumbe 12.
Ten alisema Mwenyekiti wa kamati hiyo atakuwa ni Majid Suleiman na Makamu wake Mustapha Urungo na Urio Edward ni Katibu. Ten aliwataja wajumbe wengine kuwa ni Rodgers Gumbo, Omary Chuma, Yanga Makoga, Lameck Nyambaya, Samuel Lukumayi, Hussein Nyika, Edgar Mutani, Leonard Chinganga na Yusuph Mohamed.
Ten alieleza kamati hiyo imeundwa na Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga na inaanza kazi mara moja kuhakikisha Yanga inafanya vyema katika mechi zake za Ligi Kuu. Sanga amekaririwa akisema ana imani kamati hiyo itafanya vyema kazi yake na kutimiza malengo yao kuwa bingwa tena msimu huu.
“Ni kamati ya kawaida ambayo ina lengo la kuhakikisha ubingwa unaendelea kubaki Jangwani kwa msimu wa nne na kufanya vizuri katika Ligi ya Mabingwa Afrika,” alisema. Yanga inaendelea na usajili kuimarisha safu yake na jana ilikamilisha usajili wa kiungo wake wa kimataifa Mzimbabwe, Thabani Kamusoko.
Wakati huohuo, Simba wameimarisha safu ya ulinzi baada ya kumsajili kipa Said Mohamed ‘Nduda’ aliyeng’ara michuano ya Cosafa kwa mkataba wa miaka miwili. Usajili wake unaifanya Simba msimu ujao iwe na makipa watatu wote wapya. awali ilimsajili kipa Aishi Manula wa Azam na Emmanuel Mseji wa Mbao FC ya Mwanza.
Simba pia imemsajili Erasto ambaye awali alikuwa akichezea Azam FC. Nyoni kama alivyo Manula na Nduda wako Taifa Stars. Waliondoka na Stars jana kwenda Kigali, Rwanda kwa mechi ya marudiano ya kufuzu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ligi za ndani (Chan).
No comments:
Post a Comment