Stars yajiweka pabaya
TIMU ya soka ya Taifa, Taifa Stars jana ilijiweka vibaya kwenye harakati za kufuzu kombe la mataifa Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN) baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 na Rwanda katika mechi iliyochezwa kwenye uwanja wa CCM Kirumba mjini hapa.
Matokeo yanaiweka pabaya Stars kwani sasa ili kufuzu inahitaji ushindi wowote katika mechi ya marudiano itakayochezwa Kigali Rwanda mwishoni mwa wiki ijayo. Timu itakayoshinda mechi hiyo itacheza na mshindi kati ya Sudan Kusini na Uganda ambazo jana zilitoka suluhu mjini Juba.
Rwanda ilikuwa ya kwanza kupata bao la kuongoza lililofungwa na Dominique Nshuti katika dakika ya 17. Stars haikuwa inacheza vizuri katika dakika hizo na hivyo kocha wake mkuu, Salum Mayanga alilazimika kufanya mabadiliko ambapo alimtoa Shomari Kapombe aliyeumia na nafasi yake kuchukuliwa na Boniphace Maganga katika dakika ya 18.
Mabadiliko hayo kidogo yalizaa matunda na dakika ya 33, Stars ilisawazisha bao hilo kupitia kwa Himid Mao aliyefunga kwa mkwaju wa penalti. Mwamuzi wa mchezo huo, Alier James wa Sudan Kusini aliamuru ipigwe penalti baada ya mchezaji wa Rwanda, Rucogoza Aimambe kunawa shuti lililopigwa na Gadiel Michael.
Bao hilo kidogo lilileta uhai kwa Stars ambapo sasa ikawa ikipeleka mashambulizi kwa zamu na wenyeji wake na dakika ya 45 nusura Maganga aipatie bao Stars baada ya kuachia shuti kali lakini kipa wa Rwanda, Ndalishime Erick akapangua.
Katika mechi ya jana, Stars ilionekana kuwa dhaifu katika safu ya ushambuliaji iliyokuwa chini ya mshambuliaji mpya wa Simba, John Bocco. Aidha mchezo huo ulitawaliwa na ubabe mwingi hasa katika kipindi cha pili ambapo wachezaji wa pande zote walionekana kutoleana lugha za maudhi.
Michuano hiyo ilianziShwa kwa mara ya kwanza mwaka 2009 ilipofanyika Ivory Coast na Stars kuwa miongoni mwa timu za kwanza kufuzu. Tangu wakati huo haijafuzu tena na hivyo inajaribu tena bahati yake katika fainali hizo za mwakani zilizopangwa kufanyika Kenya.
Stars: Aishi Manula, Shomari Kapombe, Gardiel Michael, Nurdin Chona, Salim Mbonde, Erasto Nyoni, Simon Msuva, Himid Mao, John Bocco/ Stahmili Mbonde, Muzamil Yassin, Shiza Kichuya.
Rwanda: Ndayishimiye Eric, Marcel Mubumbyi/Latif Bishira, Bizimana Djihad, Dominique Savio Nshuti/Innocent Nshuti, Emmanuel Imanishimwe, Iradukunda Eric, Manzi Thierry, Mico Juastin/Kayumba Soter, Yannick Mukunzi, Nsabimane Aimable na Rucogoza Aimable.
No comments:
Post a Comment