Saturday, July 22, 2017

Makandarasi wazembe wafukuzwe - JPM

RAIS John Magufuli ameitaka Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi kuwachukulia hatua wakandarasi waliopewa miradi ya barabara, lakini wakashindwa kuikamilisha kwa wakati.
Akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa mradi wa barabara ya kiwango cha lami kutoka Nyakanazi wilaya ya Biharamulo mkoa Kagera hadi Kakonko mkoani Kigoma, Rais Magufuli alisema serikali haitakubali kuona wakandarasi wanafanya kazi wanavyotaka badala ya kuzingatia mikataba yao.
Amemuagiza Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na uchukuzi Profesa Makame Mbarawa kutokuwa mpole, badala yake kuwafukuza makandarasi watakaofanya kazi ovyo ovyo au kuchelewesha kumaliza kazi walizopewa.
Sambamba na hilo, amemuagiza Mkandarasi kampuni ya Nyanza Roads Work kujipanga kuhakikisha anafanya kazi usiku na mchana ili kumaliza barabara hiyo haraka, huku akitaka mkandarasi huyo kulipwa madai yake kulingana kazi ambazo ameshafanya hadi sasa.
Alisema serikali yake imedhamiria kuufungua mkoa wa Kigoma kwa kukamilisha miradi ya barabara ya kiwango cha lami kutoka Kigoma hadi Nyakanazi na Kigoma hadi Tabora, barabara ambazo pia ni kiunganishi cha mikoa ya magharibi na mikoa ya kanda ya ziwa pamoja na kuunganisha na nchi za maziwa makuu.
Alisema serikali inakusudia kuona Watanzania wakisafiri kutoka Nyakanazi wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera hadi Dar es Salaam kwa kutumia bajaji. Awali, Profesa Mbarawa alisema mradi huo utagharimu Sh bilioni 48.5 zilizotolewa na serikali ambapo kati ya fedha hizo, Sh bilioni 45.5 zitatumika kwa ujenzi, bilioni 2.4 usimamizi huku kiasi cha Sh milioni 100 ni kwa ajili ya kulipa fidia.
Alimweleza Rais Magufuli kuwa, mkandarasi wa barabara hiyo amekuwa akitekeleza kazi ya ujenzi polepole na kwamba serikali inakusudia kutoipa tena kampuni hiyo miradi ya barabara kama hatajirekebisha.

No comments:

Post a Comment