Friday, July 7, 2017

Rais wa TFF, Jamal Malinzi na wenzake wasomewa mashitaka 28


Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi pamoja na wenzake wamesomewa mashitaka 28 huku yakiwemo ya kughushi na utakatishaji fedha zaidi ya dola za Marekani 300,000.

Wengine katika kesi hiyo ni Katibu Mkuu wa TFF, Mwesigwa Selestine na Nsiande Mwanga ambao wamesomewa mashitaka yao leo (Alhamisi) mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Kati ya Mashitaka hayo Malinzi pekee anakabiliwa na mashitaka 22 ya kughushi risiti mbalimbali zinazoonesha kuwa aliikopesha TFF fedha kwa nyakati tofauti, mashitaka mengine yanawahusu Selestine na Nsinde huku shitaka moja likiwahusu wote.

Akisoma hati ya mashitaka Wakili Mwandamizi wa Serikali, Nassoro Katuga kwa kusaidiana na Wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Leornad Swai amedai kwa nyakati tofauti washtakiwa hao walitenda makosa hayo ndani ya jiji la Dar es Salaam.

Hata hivyo, upande wa jamhuri uliomba kesi hiyo ihairishwe kwa madai upelelezi haujakamila, ambapo Hakimu Mashauri aliahirisha kesi hiyo hadi Julai 03, mwaka huu.

Baada ya kesi hiyo kuahirishwa gari ya polisi iliwasili saa 10:26 na kuwachukua watuhumiwabhao pamoja na Rais wa Simba, Evance Aveva na Makamu wa Rais, Geofrey Nyange "Kaburu" ambao na wao wanakabiliwa na kesi ya utakatishaji fedha dola za Marekani 300,000.

No comments:

Post a Comment