Taifa Stars kufa au kupona Rwanda
TIMU ya soka ya Taifa Stars inashuka dimbani leo Jijini Kigali, Rwanda kuwania kufuzu kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (Chan) dhidi ya Rwanda, Amavubi.
Taifa Stars inajitupa uwanjani ikiwa imeongezewa nguvu na mshambuliaji wa Yanga, Simon Msuva aliyeachwa wakati Stars ilipoondoka Dar es Salaam. Mchezo huo ni wa marudiano baada ya timu hizo kutoka sare ya 1-1 katika mchezo wa kwanza uliofanyika Jumaosi iliyopita Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
Mchezo wa leo ni muhimu kwa Stars kwani inahitaji ushindi au sare ya mabao 2-2 isonge mbele na kucheza ama na Uganda au Sudan Kusini ambazo zinarudiana pia. Katika mchezo wa awali uliofanyika Sudan Kusini, zilitoka suluhu. Sare ya 1-1 inaiweka Taifa Stars katika wakati mgumu kwani zikitoka suluhu leo au kufungana au ikafungwa, itatolewa.
Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Salum Mayanga anatakiwa kupanga kikosi imara ambacho kitacheza kwa bidii na kuibuka na ushindi katika mchezo huo wa leo. Msuva aliyebaki kushughulikia mipango ya kujiunga na timu moja ya Morocco, anatarajiwa kuiongezea Stars nguvu na hivyo kutoa matumaini ya ushindi.
Hata hivyo, Taifa Stars inatakiwa kuacha ndoto za kutoka sare kwani kufanya hivyo kutaikosesha nafasi ya kuelekea kufuzu kwa mara ya pili kwa fainali hizo baada ya kucheza kwa mara ya kwanza mwaka 2009 Ivory Coast. Katika fainali hizo, Tanzania ilipangwa Kundi A na Senegal, wenyeji Ivory Coast, Zambia na Senegal.
Ilimaliza ikiwa ya tatu kwa kuwa na pointi nne. Zambia na Senegal zilifuzu kwa hatua ya robo fainali baada ya kumaliza nafasi ya kwanza na pili kila moja ikiwa na pointi tano zikitofautiana mabao.
No comments:
Post a Comment