Ewura yakoleza agizo mafuta
ZIKIWA zimebaki takribani siku tisa kwa wenye vituo vya mafuta kutekeleza agizo la Rais John Magufuli la kufunga mashine za kielektroniki za ukusanyaji wa kodi, Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) imekoleza amri hiyo kuwa inasimamiwa na sheria ikiwemo ya kodi na mafuta.
Aidha, Ewura imesema katika taarifa yake kwa umma iliyotolewa jana kuwa, baada ya siku hizo 14, yeyote atakayekaidi amri hiyo ya Rais kwa wenye vituo vya mafuta, hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake. Julai 19, mwaka huu, Rais Magufuli alitoa siku 14 kwa wamiliki wa vituo vya mafuta nchini, kuhakikisha kwamba wanafunga mashine za EFDs na alionya kuwa watakaoshindwa kufanya hivyo, watahatarisha biashara zao.
Aliwataka wakuu wa mikoa na wilaya, kufuatilia na kusimamia jambo hilo kwa karibu. Alitoa agizo hilo akiwahutubia wananchi mjini Biharamulo mkoani Kagera wakati wa kuzindua barabara ya Kagoma- Biharamulo- Lusahunga yenye urefu wa kilometa 154, ambayo itaiunganisha Tanzania na nchi jirani katika Ukanda wa Magharibi kimaendeleo.
Katika hotuba yake kwa hadhara hiyo, Dk Magufuli alisema kwa muda mrefu baadhi ya wafanyabiashara nchini wasio waaminifu, wamekuwa wakiendesha vituo vya mafuta kwa kukwepa kodi na kuagiza wizara zinazosimamia hilo, ikiwemo ya Fedha na Mipango pamoja na ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, kuhakikisha vituo vyote vya mafuta nchini, vinatumia mashine hizo na kusisitiza wamiliki watakaokaidi vituo vyao vifungwe na kufutiwa leseni.
Wakati akitoa agizo hilo, karibu vituo 700 vya mafuta vilikuwa vimefungwa nchi nzima tangu kazi ya ukaguzi inayofanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ianze ukaguzi wa mashine hizo. Hata hivyo, tayari zaidi ya vituo 500 vimefunguliwa baada ya kukidhi vigezo vilivyowekwa na TRA na vingine havijafunguliwa kutokana na kushindwa kukidhi masharti hayo.
Mapema mwaka jana TRA na wafanyabiashara wa mafuta nchini walikubaliana kutumia mashine hizo katika vituo vya mafuta, lakini hadi Septemba mwaka jana, wengi hawakuwa wamefunga mashine hizo pamoja na kuwa baadhi ya matakwa yao ikiwemo kuwa na mashine moja katika pampu nne yalikubaliwa
No comments:
Post a Comment