Saturday, July 22, 2017



JPM aonya rushwa CCM


RAIS John Magufuli ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taifa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) amewataka wanaCCM kushiriki katika uchaguzi ndani ya chama hicho, lakini akawaonya kutojihusisha na rushwa.

Rais Magufuli aliyasema hayo jana wakati akiwahutubia wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Viwanja vya Posta wilayani Ngara. Rais yuko mkoani Kagera kwa ziara ya kikazi ambayo pia huitumia kuzungumza na wananchi moja kwa moja.

Mkutano wake ulirushwa moja kwa moja na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC). Mbali ya kuwataka wanaCCM kushiriki katika uchaguzi na kuwaonya wasijihusishe na vitendo vya rushwa, aliwataka wafanye uchaguzi ulio huru na haki.

Kwenye Mkutano Mkuu wa chama hicho uliofanyika Februari mwaka huu, kulifanyika mabadiliko ya Katiba ambayo pamoja na mambo mengine yalipitishwa mambo ambayo hayastahili kufanyika wakati wa uchaguzi.

Baadhi ya mambo yaliyokatazwa ni pamoja na kutangaza nia kwa kuwa kwa kufanya hivyo kunafifisha haki za wanachama wengine wasio na uwezo wa kufanya hivyo. Mambo mengine yaliyokatazwa ni kutofanya vitendo vya kushawishi vikao vya maadili, vya uteuzi au vya uamuzi, kupiga picha zinazohusiana na matukio ya uchaguzi wakati wa kuchukua fomu, kurejesha fomu na matumizi ya mitandao ya kijamii ambayo kwa mujibu wa chama hicho wanayachukulia kama njia mojawapo ya kufanya ushawishi.

Uchaguzi huo ndani ya CCM umeanzia ngazi ya Shina, matawi na utaendelea ngazi ya jimbo, wilaya, mkoa na taifa. Aidha, Rais Magufuli amewaahidi wananchi wa Ngara kuwa atalitatua tatizo la maji linalowakabili. Rais alikuwa akijibu maombi ya Mbunge wa Ngara, Alex Gashaza (CCM) aliyepewa nafasi ya kuzungumza kwenye mkutano huo.

Mbunge huyo alimweleza Rais Magufuli kuwa Ngara ina vijiji 75 na wakazi wake wanakabiliwa na tatizo la maji kwa muda mrefu sasa. Alimweleza kuwa wananchi wa Ngara wana imani na CCM na ndiyo maana kwenye Uchaguzi Mkuu uliopita walishinda udiwani kwenye kata zote 22, ubunge pamoja na kumpigia kura mgombea urais wa CCM.

Ili kupata ufumbuzi wa tatizo hilo, Rais Magufuli alimwagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Ngara kutumia bajeti ya maji ya Sh milioni 200 kwa ajili ya kutatua tatizo la maji kwa wananchi zaidi ya 20,000 wilayani humo

No comments:

Post a Comment