Thursday, July 6, 2017

‘SADC tuache utegemezi’

MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan amezitaka taasisi za kifedha za nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Uchumi Kusini mwa Afrika (SADC) kufahamu kuwa utegemezi wa misaada kutoka nje ya nchi kamwe hauwezi kuzisaidia nchi masikini kuondoka kwenye hali hiyo.
Akizungumza Dar es Salaam jana wakati wa kufungua mkutano wa taasisi za fedha kutoka nchi za SADC, Samia alisema kwa sasa nchi hizo zinatakiwa kuongeza juhudi za kuweka mikakati itakayohakikisha raslimali za ndani ya nchi husika zinachangia kikamilifu kukuza uchumi wa nchi na kukuza sekta binafsi
.
Alitoa mwito kwa taasisi za maendeleo za kifedha kuhakikisha kuwa zinashiriki kikamilifu katika kuiwezesha kifedha miradi mbalimbali ya kimaendeleo kama ujenzi wa miundombinu ambako benki nyingi zimekuwa zinakwepa.

Samia pia alisema ufadhili wa miradi mbalimbali ya kimaendeleo katika nchi mbalimbali kwa sasa unafanywa kwa kasi kubwa kwa fedha za nje pamoja na fedha za ndani kupitia taasisi za kifedha za nchi husika.

Alisema taasisi za fedha zina jukumu la kuchangia uboreshaji wa uzalishaji wa pato la taifa pamoja na kuimarisha sekta binafsi ili uwepo ushindani ambao unakidhi maendeleo endelevu yenye manufaa kwa mwanachama wa SADC na jumuiya yenyewe.

Alisema aliziomba taasisi za fedha zihusike katika kuwasaidia wafanyabiashara wa kati (SMEs) uboreshaji wa miundombinu na kuhakikisha kuwa sekta binafasi inashiriki kikamilifu katika kukuza nchi za nchi.

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashati Kijaji alisema mkutano huo ambao unazikutanisha taasisi 37 za kifedha za SADC, kutoka nchi 14 zinafanya mkutano wa mwaka hapa nchini huku kauli mbiu yao ni mkakati wa maendeleo ya viwada kwa maendeleo endelevu.

Alisema hata msisitizo katika bajeti iliyopitishwa hivi karibuni ni viwanda na akaeleza kuwa mkutano huo ni muhimu kwani hakuna viwanda kama hakuna fedha. Alisema kwa sasa nchi za SADC zinahitaji kutumia rasilimali za ndani badala ya kutegemea fedha za nje.

Alisema taasisi za fedha ni muhimu kwani hakuna viwanda bila kuwa na fedha. Aliongeza kuwa raslimali fedha ndio msingi wa viwanda na hivyo akazitaka taasisi hizo kuhakikisha zinawawezesha sekta mbalimbali zinazowezesha viwanda.

Akielezea uzoefu wa Tanzania katika ukuzaji wa viwanda, Mkurugenzi wa Ukanda wa Maeneo Huru ya Uwekezaji (EPZ), Joseph Simbakalia alisema Tanzania imefanya mageuzi makubwa katika sekta ya viwanda kwa kuondokana na viwanda vya umma badala yake kwa sasa wawekezaji binafsi ndio wanaowekeza katika sekta hiyo.

Alisema ilichofanya Tanzania ni kuandaa mazingira ya kuwekeza wawekezaji hao, ikiwemo kutenga maeneo maalumu ya uwekezaji yenye huduma zote muhimu ili mwekezaji anapokuja nchini asipate usumbufu wa kwenda kutafuta ardhi, badala yake aje tu ajenge viwanda na kuanza kuzalisha

No comments:

Post a Comment