Saturday, July 22, 2017

Majaliwa: Tutatekeleza ahadi zote za Rais

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amewahakikishia wananchi kwamba ahadi zote zilizotolewa na Rais, Dk John Magufuli katika maeneo mbalimbali nchini zitatekelezwa, hivyo amewaomba waendelee kuiamini na kushirikiana na Serikali yao.
Alitoa kauli hiyo juzi jioni wakati akizungumza na wananchi wa wilaya ya Songwe kwenye mkutano wa hadhara katika Uwanja wa Mkwajuni. Waziri Mkuu yuko mkoani Songwe kwa ziara ya kikazi.
Alisema Serikali ya Awamu ya Tano, ipo makini na imejipanga vizuri katika kutekeleza ahadi mbalimbali zilizotolewa na Rais Magufuli kama Ilani ya uchaguzi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015/2020 inavyoelekeza.
Aliyasema hayo baada ya Mbunge wa Songwe, Philipo Mulugo kumuomba awasaidie kumkumbusha Rais Magufuli kuhusu ahadi yake ya ujenzi wa barabara ya lami yenye urefu wa kilomita nne wilayani Songwe.
“Ahadi zote zilizotolewa na Mheshimiwa Rais Dokta Magufuli tutazitekeleza, ikiwemo na hii aliyoikumbusha Mheshimiwa Mulugo ya ujenzi wa kilomita nne za barabara ya lami. Tunawaomba wananchi muendelee kuwa na imani na Serikali yenu,” alisema.
Pia Waziri Mkuu alipiga marufuku wananchi kufanya shughuli za kibinadamu ndani ya meta 60 kutoka katika vyanzo vya maji. Aliwataka washirikiane katika utunzaji wa mazingira ili kuliepusha Taifa kugeuka jangwa.
Alisema ni vema wananchi wakazingatia Sheria ya Mazingira, inayozuia kufanya shughuli za kibinadamu zikiwemo za kilimo kwenye maeneo yote ya vyanzo vya maji ndani ya mita 60. Aliwaagiza wakuu wa idara kusimamia jambo hilo.
Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Chiku Gallawa akizungumzia hali ya upatikanaji wa maji katika mkoa huo, alisema watu wanaopata huduma za maji safi na salama katika maeneo ya mijini ni asilimia 42 na vijijini ni asilimia 41.6.
Alisema katika bajeti ya 2017/2018 halmashauri za mkoa huo zimetengewa Sh bilioni 7.5 kutekeleza miradi mbalimbali ya maji ikiwa ni pamoja na ujenzi wa matanki ya kuvunia maji ya mvua katika majengo ya Taasisi za Umma.

No comments:

Post a Comment