Saturday, July 22, 2017

Nyumba ya Mungu yaingiza faini mil 40/-

ZAIDI ya Sh milioni 40 zimekusanywa katika kipindi cha mwaka mmoja kutokana na faini ya makosa ya uvuvi haramu uliokuwa unafanywa wakati serikali imesitisha shughuli za uvuvi katika bwawa la Nyumba ya Mungu.
Fedha hizo zilikusanywa katika Halmashauri ya Wilaya ya Moshi na Mwanga mkoani Kilimanjaro pamoja na Simanjiro mkoani Manyara. Aidha, walikamata vyombo mbalimbali vya uvuvi na kuteketeza Makokoro 320, vyandarua 41, nyavu za kutega 129, mitumbwi 94.
Pia walikamata watuhumiwa zaidi ya 30, watatu walihukumiwa kifungo cha mwaka mmoja na kulipa faini pia ndoo 1,270 za samaki zilizokamatwa ziligawiwa kwa wananchi.
Shughuli za uvuvi katika bwawa hilo, zilisitishwa kwa mwaka mmoja kuanzia Julai Mosi, mwaka jana na kufunguliwa Julai mwaka huu ili kuruhusu samaki kuzaliana na kukua kwa sababu samaki walikuwa wanavuliwa wakiwa wadogo.
Akizungumza katika kikao cha ujirani kati ya mkoa wa Kilimanjaro na Manyara, Katibu Tawala wa Wilaya ya Simanjiro, Zuwena Jiri alisema wakati bwawa limefungwa walikuwa wanafanya doria na kufanikiwa kuzuia uvuvi usioendelevu na kuwezesha samaki kuzaliana na kukua pia wakusanya Sh milioni 21 kama fi dia za watu waliokutwa wakifanya uvuvi haramu.
Kaimu Ofi sa Uvuvi Wilaya ya Mwanga, Tito Kibona alisema baada ya doria baadhi ya wavuvi waliacha uvuvi na kuamua kuondoka eneo hilo, walikamata na kuteketeza kwa moto zana haramu za uvuvi.
Shughuli za uvuvi zimeruhusiwa, lakini watakuwa wanavua kwa muda wa miezi sita na bwawa litafungwa kuanzia Januari Mosi hadi Juni 30 kila mwaka ili kutoa muda wa samaki kuzaliana na kukua pamoja na maji kujaa ili waweze kuvua samaki wakubwa.

No comments:

Post a Comment