Taifa Stars yatolewa kiume Cosafa
Mshambuliaji wa Taifa Stars Elius Maguli
TIMU ya soka ya Taifa Stars imetolewa kwenye michuano ya kuwania Kombe la Baraza la Soka kwa nchi za Kusini mwa Afrika (Cosafa) baada ya jana kuchapwa kwa mabao 4-2 na Zambia, wana Chipolopolo katika mechi ya nusu fainali.
Stars ndiyo waliokuwa wa kwanza kupata bao la kuongoza lililofungwa na Erasto Nyoni katika dakika ya 14 kufuatia mpira wa adhabu ndogo alioupiga na kwenda wavuni moja kwa moja.
Adhabu hiyo ilitokana na beki wa Zambia kumchezea rafu Simon Msuva aliyekuwa anakwenda katika lango lao na mwamuzi kutoa adhabu hiyo iliyotumiwa vizuri na Taifa Stars. Baada ya bao hilo, Zambia walikuja juu na kufanya mashambulizi mengi lango la Taifa Stars lakini washambuliaji wake walikosa utulivu na kushindwa kutumia nafasi hizo.
Mchezo huo uliendelea kuwa na ushindani kwa kila upande kutafuta bao lakini Zambia ndiyo waliofanikiwa baada ya kufunga mabao mawili ya haraka dakika mbili kwenda mapumziko.
Taifa Stars ilielemewa zaidi baada ya kutoka kwa Nyoni baada ya kuumia kifundo cha mguu na nafasi yake kuchukuliwa na Rafael Daud. Brian Mwilu aliisawazishia Zambia dakika ya 43 kufuatia makosa ya mabeki wa Taifa Stars
.
Mabeki hao walidhani mshambuliaji huyo alikuwa ameotea. Dakika ya 45 Jastine Shonga alifunga bao la pili na kuifanya Zambia kwenda mapumziko ikiongoza kwa mabao mawili.
Kipindi cha pili, Zambia waliuanza mchezo kwa kasi na dakika ya 56 walifanikiwa kupata bao la tatu lililofungwa kwa mkwaju wa penati na Jackson Chirwa baada ya beki wa kulia wa Taifa Stars, Gadiel Michael kuushika mpira langoni.
Dakika ya 65 Shonga aliifungia Zambia bao la nne baada ya kupiga mpira wa adhabu ndogo uliomshinda kipa Aishi Manula na kujaa wavuni. Taifa Stars Stars waliendelea kupambana kusawazisha mabao hayo na juhudi zao ziliweza kuzaa matunda dakika ya 77.
Zilizaa matunda baada ya Msuva kufunga bao la pili akimalizia mpira ambao uligonga mwamba wa juu na mpira kumkuta akiwa nafasi nzuri. Taifa Stars Jumapili itacheza mechi ya kutafuta mshindi wa tatu na timu itakayofungwa katika ya Zimbabwe na Lesotho
No comments:
Post a Comment