Thursday, August 3, 2017

Wagonjwa wa moyo kwenda nje wapungua kwa 80%

IDADI ya wagonjwa wa moyo waliokuwa wakisafi rishwa kwenda nje ya nchi kwaajili ya matibabu imepungua kwa asilimia 80.
Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu wakati wa hafla ya makabidhiano ya vifaa vya chumba cha tatu upasuaji katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) kutoka Ubalozi wa Kuwait nchini.
Ummy alisema katika mwaka wa fedha 2015/2016, taasisi hiyo ilipeleka jumla ya wagonjwa 85 nje ya nchi kwa ajili ya matibabu, lakini idadi hiyo imepungua hadi kufikia wagonjwa 17 mwaka 2016/2017.
“Hii ni moja ya mikakati ya serikali ya awamu ya tano kupunguza idadi ya wagonjwa kwenda nje ya nchi kwa sababu ya matibabu na hii itapunguza gharama ambayo serikali ingeingia kwa kuwasafirisha wagonjwa kwenda nje ya nchi, naipongeza sana taasisi hii ya JKCI kwa kupunguza idadi hii,” alisema Ummy.
Aidha, Ummy ameushukuru ubalozi huo kwa msaada wa vifaa hivyo kwa ajili ya chumba hicho cha tatu cha upasuaji na kusema kuwa vitasaidia kupunguza msongamano kwa vyumba viliwi vilivyokuwa vikifanya upasuaji.
Alisema tangu kuanza upasuaji mwaka 2015 hadi 2017, jumla ya wagonjwa 713 walifanyiwa upasuaji na kati yao asilimia 61 ni watoto na watu wazima asilimia 39.
“Kuongezeka kwa chumba cha tatu cha upasuaji tunatarajia kufanya upasuaji zaidi ingawa tutakuwa bado na changamoto ya kukosa mashine ya kufanya upasuaji bila kufunua moyo (heart lung bypass),” aliongeza Ummy na kuipongeza taasisi hiyo kwa utendaji wake ulioifanya kuwa bora hadi kuifanya Malawi kuitumia kwa kuwapa rufaa wagonjwa wake kuja kutibiwa katika taasisi hiyo.
Kwa upande wake, Balozi wa Kuwait nchini, Jasem Al-Najem alisema vifaa hivyo vimegharimu Sh milioni 325, na kwamba ubalozi huo umeamua kutoa msaada huo ikiwa ni kuisaidia serikali katika kukabiliana na changamoto zinazoikabili sekta ya afya

No comments:

Post a Comment