Saturday, February 10, 2018

Msigwa abanwa, atakiwa kuwasilisha vielelezo bungeni



Msigwa abanwa, atakiwa kuwasilisha vielelezo bungeni

Naibu Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson amemwagiza Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini, Peter Msigwa (Chadema) kuwasilisha nyaraka zinazodai kuwa na habari mbaya za rushwa katika Mkataba wa Makubaliano (MoU) kuhusu ya utengenezaji wa pasipoti za kielektroniki uliozinduliwa hivi karibuni.
Msigwa alidai bungeni jana kuwa, chama chake cha Chadema, kimepata nyaraka zinazoonesha gharama ya pasipoti za kielektroniki ambayo ilizinduliwa na Rais John Magufuli, hazikufuata taratibu za ununuzi wa haki.
Wakati wa uzinduzi wa pasipoti za kielektroniki, serikali ilibainisha kuwa hati hizo zitatolewa kwa gharama ya Sh 150,000 ambazo zitadumu kwa miaka 10. Mradi wa pasipoti za kielekroniki unatekelezwa na Ireland na Kampuni HID ya Marekani kwa gharama ya Dola za Marekani milioni 57.82.
Hata hivyo, Msigwa alibua suala la mradi huo wakati wa kujadili taarifa ya utekelezaji wa shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama katika kipindi cha Januari 2017 hadi Januari 2018.
“Wakati mfumo huu unazinduliwa, hatukuambiwa ikiwa ni pasipoti za kielektroniki au uhamiaji. Umma unadhani unahitaji kuwambiwa kipi ni kipi. Tunahitaji ufafanuzi kwenye suala hili,” alisema.
Tuhuma hizo zilimfanya Naibu Spika, Dk Ackson kuingilia kati na kumtaka mbunge huyo kupeleka nyaraka kwenye Kamati ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge yenye uwezo wa kuchunguza na kutoa ushauri hatua gani zichukuliwe kuhusu jambo hilo.
Akijibu hoja hiyo, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Mwigulu Nchemba alimtaka Msigwa kutopotosha umma kwani mfumo wa pasipoti za kielektroniki haulengi hati ya kusafiria pekee, bali pia unajumusha utoaji huo wa viza za kielektroniki (e-Visa), vibali vya ukaazi vya kielektroniki (e-Permit) na udhibiti wa mipaka wa kielektronikia.
Hivi karibuni, Idara ya Uhamiaji ilibainisha ufisadi wa Sh bilioni 400, zilizolengwa kuhujumiwa kupitia zabuni ya utengenezaji wa pasipoti mpya za kielektroniki za kusafiria. Pia lilibainisha hujuma mpya ya kuwepo kwa kundi la wanasiasa linalotumiwa kufanya siasa chafu za kudhoofisha mchakato wa utoaji hati mpya za kielektroniki za kusafiria na kuwataka kuacha kufikiria maslahi yao na kutanguliza mbele maslahi ya Taifa.
Hivi karibuni, Rais Magufuli wakati akizindua hati mpya za kusafiria za kielektroniki, alisema kumekuwapo na wahujumu wa mchakato huo, ambao walipanga kufisidi Sh bilioni 400, bila mafanikio