Friday, October 20, 2017
MBARAKA, SURE BOY "BAMPA TO BAMPA" TUZO YA MWEZI AZAM FC
MBARAKA, SURE BOY "BAMPA TO BAMPA" TUZO YA MWEZI AZAM FC
MABARA |
Kiungo wa Azam FC, Salum Abubakar ‘Sure Boy’ na mshambuliaji, Mbaraka Yusuph wameingia katika vita ya kuwania tuzo ya mchezaji bora wa mwezi Septemba ambayo hutolewa kila mwezi klabuni hapo.
Majina hayo ya wachezaji wa Azam yamependekezwa na viongozi wa timu hiyo akiwemo kipa wa kigeni Razark Abalola raia wa Ghana miongoni mwa wachezaji watatu walioingia katika kinyang’anyiro hicho.
Ofisa Habari wa Azam FC, Jaffari Idd alisema kuwa, jopo la viongozi wamepitisha majina hayo ambayo yatapigiwa kura kwa kuzingatia kiwango cha mchezaji na nidhamu kwa jumla.
“Kama ulivyo utaratibu wa Azam FC, jopo la viongozi wamepitisha majina matatu ya wachezaji akiwemo Sure Boy, Mbaraka na kipa Razark kwa ajili ya kuchuana katika tuzo ya Septemba ambapo mashabiki wa soka ndiyo watakaopata nafasi ya kupiga kura kupitia mitandao ya kijamii na atakayepata kura nyingi ndiyo atakayeibuka mshindi.
“Vigezo vitakavyozingatiwa ni nidhamu ya mchezaji, uwezo wa kujituma uwanjani na vitu vingine, vitu vyote hivyo vitaamuliwa na mashabiki kama ilivyo mwezi uliopita tulipompata mchezaji bora wa mwezi wa nane ambaye alikuwa Yakub Mohamed, hivyo tunawaomba wadau kufuatilia mechi zetu za Azam kisha kupiga kura na si kubuni,” alisema Jaffari.
Aidha, wachezaji hao walipoulizwa kuhusiana na tuzo hiyo walieleza kuwa, wamefurahishwa na hatua hiyo iliyochukuliwa na viongozi wao huku kila mmoja akiahidi kuitwaa tuzo hiyo na kudai kuwa itawaongezea morali ya kujituma zaidi katika kila mechi.
Thursday, October 19, 2017
KUKOSEKANA KWA KAMUSOKO; ALICHOSEMA LWANDAMINA HIKI HAPA...
KUKOSEKANA KWA KAMUSOKO; ALICHOSEMA LWANDAMINA HIKI HAPA...
Kocha Mkuu wa Yanga, George Lwandamina amefunguka kuwa hakuna pengo lolote ndani ya kikosi chake licha ya kuwakosa baadhi ya wachezaji nyota wa timu hiyo, Thabani Kamusoko na Donald Ngoma ambao ni majeruhi.
Kocha huyo amesema hayo wakati wachezaji hao Jumamosi iliyopita walishindwa kuwa sehemu ya kikosi cha Yanga ambacho kilishuka dimbani kumenyana na Kagera Sugar ambao walishinda kwa mabao 2-1, kwenye mchezo wa ligi kuu uliopigwa Uwanja wa Kaitaba, Bukoba.
Kamusoko yuko nje akisumbuliwa na kifundo cha mguu (enka) ambapo atazikosa mechi zote za timu hiyo Kanda ya Ziwa dhidi ya Kagera Sugar na Stand United, huku Ngoma akisumbuliwa na majeraha ya goti.
Lwandamina amesema kwake haoni shida ya kutokuwa na wachezaji hao kwenye kikosi hicho kutokana na uwepo wa wachezaji wengine ambao wanaifanya kazi vizuri na kupata matokeo.
“Huwezi kusema kwamba kuna pengo la Ngoma au Kamusoko kwa sababu unapozungumzia timu ni juu ya watu wote ambao wapo na hali ya umoja iliyopo na siyo suala la mchezaji mmoja pekee, ndiyo maana utaona hatukuwa nao lakini tumepata matokeo mazuri.
“Kwangu hakuna pengo la mchezaji yeyote yule kutokana na waliopo kuifanya kazi vizuri na matokeo tunapata, kuna zaidi ya wachezaji 20 hapa sasa wanapokosekana wachezaji wawili au watatu hilo siyo pigo hata kidogo kwetu, kwani ninachukua mbadala wake na ninamtumia,” alisema kocha huyo wa zamani wa Zesco United ya Zambia.
SOURCE: CHAMPIONI
Subscribe to:
Posts (Atom)